Translate

Friday, March 20, 2015

CCM iruhusu wagombea wajitangaze rasmi

Inashangaza kwamba kufikia leo hii, CCM bado inawazuia wanachama wake kutangaza kugombea urais.
Chini chini, idadi ya wanaotaka kugombea nafasi hii inaongezeka. Wengine wanataka wenyewe, wengine wanasakiziwa.
Ukweli ni kwamba, ingawa nafasi ya urais ni moja tu, wanaoitamani ni wengi kupindukia.
Vyama vingine vimebaki kimya, si kwamba vinazuia mtu kujitangaza labda ni mbinu za kutaka kusubiri kwanza kuona chaguo la CCM ili wajipange. Ila bado hatujasikia tamko la kuwazuia wanachama wa upinzani kujitokeza kugombea kama tunavyosikia kutoka CCM.
Unaweza kuiba, wakafumba macho, unaweza kukosa uzalendo, wakafumba macho, unaweza kushindwa kuwajibika wakafumba macho, unaweza kutoa roho ya mtu wakafumba macho, lakini ukitangaza kugombea urais kabla ya muda, unawekwa kifungoni. CCM wanashangaza!
Ukali wanaouonyesha kwa watu wanaojitangaza mapema unatisha. Wangekuwa wakali kwa mambo mengine ya msingi, Taifa letu lingekuwa mbele zaidi.
Mwaka jana, CCM iliwafungia wanachama wake sita waliojitokeza kujitangaza kugombea.
Wakapata adhabu ambayo hadi leo ni kama inaendelea maana, hakuna uwazi. Katika dunia ya leo ya sayansi ya teknolojia, bado mambo yanaendeshwa kama uchawi vile.
Tukihesabu siku, zinakwenda. Tungependa kuwafahamu wagombea, tungependa kuwahoji na kuyachunguza maisha yao, kuchunguza imani zao za mambo mbalimbali.
Ni muhimu kufahamu mtu anayetaka kugombea uongozi wa juu katika Taifa anaamini nini? Ana itikadi gani? Anafuata sera gani? Ni mzalendo au ni kibaraka? Yote haya ni muhimu kufahamika mapema.
Ushawishi wa wananchi
Wagombea wa CCM, hawatoki mwezini. Ni watu wanaoishi kwenye jamii yetu. Tunawafahamu. Hivyo CCM, haiwezi kukwepa ushawishi wa wananchi.

No comments: