Translate

Saturday, March 21, 2015

Mariana: Nilikeketa mabinti 20 wakazimia, sasa naelimisha jamii



KWA UFUPI
Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 130 katika nchi 29 barani Afrika na Mashariki ya Kati wameshafanyiwa ukeketaji
“Sitaisahau hii siku maishani mwangu, kutokana na mawazo, hofu na kero niliyoipata kutoka kwa mume wangu, watoto na hata majirani zangu ambao baadhi walikuwa wakisema eti nimeua wasichana 20 baada ya kuwakeketa.
Ilikuwa alfajiri nilipoamka na kuanza kazi ya kuwakeketa wasichana hao 20 nilioletewa na wazazi wao. Nilipoanza kuifanya hiyo kazi huku nikiwa tayari nimeshawakeketa wasichana 12, walianza kuishiwa nguvu na baadhi yao walikuwa wakitokwa na damu nyingi tofauti na wasichana wengine ambao nilikuwa nikiwakeketa kabla yao.
Cha kusikitisha zaidi, nilipomaliza kuwakeketa wote 20, hali zao zilikuwa mbaya na baadhi walizimia, huku damu nyingi zikiendelea kuwatoka.
Niliogopa sana…sikujua la kufanya lakini namshukuru Mungu alinihurumia, mabinti wale baadaye walizinduka na kupata fahamu. Tangu siku hiyo, niliapa kuwa sitafanya tena kazi hiyo ya ukeketaji maana niliona sasa kuna hatari ya kuja kuua.”
Hiyo ni kauli ya ngariba mstaafu Mariana Ndama (66), mkazi wa Kijiji cha Ikungi mkoani Dodoma.
Kwa Mariana, tukio hilo alilichukulia kuwa si la kawaida na hata aliwaza kuwa huenda wenzake wamemchezea mchezo mchafu wa kuroga kwa nia ya kutomtakia heri katika kazi yake hiyo.
Anasema ajali hiyo ya ukeketaji ilikuwa ya kwanza kwake tangu alipoanza kazi hiyo mwaka 1965,  katika Kijiji  cha Puma mkoani Dodoma.
Hakumbuki idadi halisi ya wasichana aliowakeketa kwa sababu hakuwa anatunza kumbukumbu, bali anakadiria kuwa ni zaidi ya 1,000.
“Nilikuwa nakeketa wasichana kuanzia watano mpaka 30 kwa wakati mmoja, hawa waliletwa nyumbani kwangu au wakati mwingine niliwafuata katika vijiji vyao. Niliitwa kwenda kufanya shughuli hiyo,” anasema.
Mariana anasema kilichomsukuma kuwa ngariba mkeketaji ni kwanza, kupunguza gharama za kuwalipa mangariba, wakati huo ilikuwa  Sh2 kwa kila msichana.
Pili,  alivutiwa kufanya kazi hiyo baada ya kuona bibi yake akiifanya, akisema faida yake aliona inaweza kumletea sifa ya ujasiri na kujulikana pia.
“Nilianza kufanya majaribio kwa watoto wangu mwenyewe ili kunijengea ujasiri wa kutowaonea huruma wasichana wengine. Nilipoona nimefanikiwa kuwakeketa binti zangu wawili ambao sasa wana wajukuu… basi  nikaona ninaweza na kazi yangu ikawa rahisi kuwakeketa wasichana kwa sababu nilishakomaa. Sikuwa na huruma hata kidogo nilipokuwa nikiifanya kazi hiyo,” anasema.

No comments: