Dodoma. Leo, Serikali itawasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 kwa hati ya dharura unaoorodhesha adhabu mbalimbali, ikiwamo ya faini ya Sh50 milioni au kifungo kisichopungua miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.
Baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo ni kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za utupu za watoto.